MAKATAZO YA KISHARI`AH KWA WANAWAKE
Imekusanywa Na: Abu Faatwimah
Katazo La Kutokuwa Na Shukurani [Kukanusha] Ihsaan
Huu
dada yangu Muislamu ni uwanja mwingine wenye hatari kubwa, na kwa
bahati mbaya ni kuwa wengi miongoni mwa wanawake kwa masikitiko makubwa
wameuingia na kuamua kuwa ni katika sehemu zao za kuishi na kutafuta
kuridhiwa au kupewa ruhusa ya kwenda watakapo hata kama ni kwenye maasi
na pasipo mridhia Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Wanawake
wengi siku hizi wanapotaka jambo ambalo wanaelewa kuwa mume hatoridhika
nalo au halipendi au hata wakati mwingine hayuko tayari nalo kwa sababu
moja au nyingine au hata kama hataki ni haki yake; huwa silaha yao
kubwa ya kutaka wakubaliwe walitakako kusema usemi wao mashuhuri na
wenye kupendeza katika midomo yao: Sikupata kuiona kheri hata siku moja kutokana nawe; yote kwa kuwa amekataliwa siku hiyo alitakalo au amezuiliwa kufanya alitakalo au kwenda atakapo.
Mke
ni mwepesi wa kusahau au kujisahaulisha kwa alitakalo na kwa wakati
autakao na wakati huo huo ni mwepesi kukumbuka kila alitakalo hasa hasa
yasiyokuwa na faida wala maana yoyote katika Dini wala dunia yake.
Mke
hununa na kuusawijisha uso wake kwa kuwa tu mume amemkatalia jambo au
amemueleza jambo ambalo mke hayuko tayari au hataki kulisikia kwa kuwa
ana lake ameliweka na analiona ndio sawa; pengine keshapanga na shoga
zake walifanye au wende, hivyo huona kuwa shoga zake watamuona kuwa hana
kauli mbele ya mumewe au hapendwi au hana ujanja na mbinu za kumpelekea
mume amkubalie na kumridhia kwa alitakalo; hivyo hugeuka na kuwa kama
asiyekuwa na akili yake wakati huo na kutoa kauli kama hizo na nyingine
mbaya zisizokubalika, kama vile mke kumwambia mumewe unanihangaisha tu
kwa kuwa amemtaka huduma na kadhalika; kauli zenye kumpelekea mume
kufikia wakati mwingine kujiuliza masuala mengi tu likiwemo hili, hivyo
ni kweli hakuwahi kumtendea jema mkewe hata mara moja katika miaka yao
yote waliyokaa kama mke na mume?! Hivyo ni kweli kwa kumtaka mkewe
amtekelezee huduma fulani [kama vile kumtayarishia chakula kumsogezea
maji] ni kweli huwa anamuhangaisha?
Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema kwamba Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Nimeonyeshwa Moto, tahamaki wengi watu [wakaazi] wake
ni wanawake; wanakanusha; pakasemwa: “Wanamkanusha Allaah!” Mjumbe wa
Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:
“Wanakanusha waume zao na wanakanusha ihsaan [wanazofanyiwa na waume
zao]; lau ukimfanyia ihsaan mmoja kati yao dahr [milele], kisha akaja
akaona kitu kidogo kwako, basi husema: Sikupata kuiona kheri yoyote katu [hata siku moja] kutokana nawe” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, kitabu cha Iymaan, mlango wa Kufraanil ‘Ashiyrah na kufr duwna kufr, Hadiyth namba 28].
Na kutoka kwa Jaabir (Radhiya Allahu ‘anhu) amesema kwamba nilishuhudia Swalaah pamoja na Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) siku ya ‘Iyd; alianza (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na
Swalaah kabla ya khutbah, kisha akasimama huku akimtegemea Bilaal
(Radhiya Allahu ‘anhu); hadi alipowaendea wanawake akawawaidhi,
akawakumbusha, na akawaamrisha kuwa na taqwa ya Allaah; akasema: “Toeni Swadaqah, akataja mambo katika mambo ya Jahannam [ikiwemo kuwa wakaazi wake wengi ni wanawake],
akasimama mwanamke... akasema: Kwa sababu gani ee Mjumbe wa Allaah?
Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:
Kwa sababu nyinyi mnaeneza malalamiko na laana; na mnakanusha ‘ashiyrah”
[Imepokelewa na Maalik, katika Muwattwaa, Kitabu cha Swalaah ya Kusuwf,
mlango wa al ‘amali katika Swalaah ya Kusuwf, Hadiyth namba 442].
Dada
yangu Muislamu kutokuwa na shukurani au kukanusha ihsaan ndio kukanusha
neema kwenyewe huko; nako ni kukanusha yale yote aliyokutendea na
kukutekelezea mumeo yakiwemo matumizi ya kila siku na kadhalika.
Katazo La Kukaa Faragha Na Asiye Kuwa Maharim
Uislamu
unapendelea mahusiano yoyote yale baina ya mwanamme na mwanamke wenye
kuweza kuoana yawe na mipaka na udhibiti wenye kuchunga heshima na
kujiweka mbali na yenye kuweza kutokea ambayo ni haramu pindi tu wawili
hawa wenye jinsi tofauti na wenye maumbile yaliyopambiwa
na kupandikizwa kupenda matamanio ya kila mmoja kutaka kuelemea kwa
jinsi iliyo tofauti na yake watapokuwa faragha; Allaah Anasema:
“Watu
wamepambiwa kupenda matamanio ya wanawake, na wana, na mirundi ya
dhahabu na fedha, na farasi asili, na mifugo, na mashamba. Hayo ni
starehe ya maisha ya duniani; na kwa Allaah ndio kwenye marejeo mema” [Aal-‘Imraan 3: 14].
Ni
katika yenye kupendwa na wengi ukaaji wa faragha kwa wawili wenye
jinsiya tofauti na wenye uwezo wa kuoana huku wakielewa fika kuwa ukaaji
wao huo unaweza kuwapelekea kutenda kila lililokatazwa na Allaah na
Mtumewe litalo wapelekea kufikia kuwa wenye kustahiki adhabu ilyowekwa
na Allaah hapa duniani au huko Aakhirah.
Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allahu ‘anhu) amesema kwamba alimsikia Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akihutubia kwa kusema: “Asikae faragha mwanamme na mwanamke isipokuwa [mwanamke huyo] awe na maharimu wake...” [Imepokelewa
na na Al-Bukhaariy, kitabu cha Tafsiyr ya Qur-aan, Suwrat Qul A’uwdhu
Birabbil Falaq, Hadiyth namba 4860; na Muslim, kitabu Kitabu cha Hajj,
mlango wa Safari ya mwanamke pamoja na Maharimu wake kwenda Hajj,
Hadiyth namba 2399].
Na kutoka kwa Jaabir bin ‘Abdillaah (Radhiya Allahu ‘anhu) amesema kwamba Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mwenye kumuamini Allaah na Siku ya Mwisho asiingie katika Hammaam [mahodhi ya kuogea] isipokuwa awe amevaa miizar [shuka]; na mwenye kumuamini Allaah na Siku ya Mwisho asimuingize khaliylah wake [mkewe] katika Hammaam; na
mwenye kumuamini Allaah na Siku ya Mwisho asikae kwenye meza yenye
kunywewa ulevi; na mwenye kumuamini Allaah na Siku ya Mwisho asikae
faragha [peke yake] na mwanamke asiyekuwa na maharimu wake pamoja naye, kwani watatu wao huwa shaytwaan” [Imepokelewa na Ahmad, katika Musnad, Musnad Kumi waliobashiriwa Jannah, iliyobaki Musnad Mukthiriyna katika Swahaba (Radhiya Allahu ‘anhum), Hadiyth namba 14356].
Na katika desturi yenye kwenda kinyume na mafundisho ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni hii desturi ya watu kukaa faragha na shemeji zao; aliulizwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu
shemeji na majibu yalikuwa kwamba shemeji ndio hasa hatari [mauti]
kubwa kwa kukaa faragha na mke wa ndugu yake, kwani yeye huwa na nafasi
kubwa asiyokuwa nayo mtu mwingine wa nje asiyekuwa shemeji; Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:”Tahadharini kuwaingilia [kuingia majumbani mwao] wanawake; akasema mtu mmoja miongoni mwa Answaar: Ee Mjumbe wa Allaah, vipi kuhusu Hamuu [shemeji]?! Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: Hamuu ni mauti. [“Hamuu”
Katika hali hii kunamaanishwa ndugu za mume (wa kiume). Haafidh Ibn
Hajar (Rahimahu Allaah) kasema: "Atw-Twabariy kasema: "Maana yake ni
kwamba
kuwepo kwa mwanamke katika nyumba au chumba na kaka wa mume au binamu
ya mke wawili peke yao ni kama kifo, kwa kuwa Waarabu huzoea kuita kila
kitu chenye hatari “kifo”]. [Imepokelewa
na Al-Bukhaariy, kitabu cha Ndoa, mlango asikae faragha mwanamme na
mwanamke isipokuwa awepo maharimu, Hadiyth namba 4859; na Muslim, katika
Kitabu cha Salamu, mlango uharamu wa kukaa faragha na mwanamke
asiyekuwa maharimu wako na kuingia nyumbani kwake, Hadiyth namba 4044.].
Ni vyema ieleweka kuwa shemeji wa mtu, binamu ya mke wa mtu si miongoni mwa Maharimu zake kwa kuwa wao wanaweza kumuoa hali kadhalika wengi wa jamaa za mume si Maharimu wa mke.
Pia
katika kawaida zenye kwenda kinyume na mafundisho ya Mtume (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni hii desturi ya watu kulala
kwenye nyumba za wanawake wajane; kutoka kwa Jaabir bin ‘Abdillaah (Radhiya Allahu ‘anhu) amesema kwamba Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Asilale mwanamme yeyote yule kwa mwanamke mjane (na katika Riwaayah): [katika nyumba] isipokuwa awe mwenye kumuoa au maharimu wake.” [Imepokelewa
na Muslim, katika Kitabu cha Salaam, mlango uharamu wa kukaa faragha na
mwanamke asiyekuwa maharimu wako na kuingia nyumbani kwake, Hadiyth
namba 4043.].
Na
katika mazoea na mila walizonazo watu zenye kwenda kinyume na
mafundisho ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni haya
mazoea ya kwenda au kuingia kwenye nyumba za watu ambao waume hawapo na
kukaa kupiga domo [soga] au kutoa stori za kweli na uongo na mke wa
mtu.
Kutoka kwa ‘Abdullaah bin ‘Amru bin Al-‘Aasw (Radhiya Allahu ‘anhu) amesema kwamba: “Watu
kutoka bani Haashim waliingia kwenye nyumba ya Asmaa bint ‘Umays; basi
akaingia Abu Bakr (Radhiya Allahu ‘anhu)... alipowaona hao watu
hakufurahi [alichukizwa], akamueleza Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam); Abu Bakr (Radhiya Allahu ‘anhu) akasema: Sikuona isipokwa kheri. Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Hakika Allaah Amemuepusha [Asmaa]
na hayo. Kisha akasimama Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa
aalihi wa sallam) kwenye minbar akasema: Asiingie mwanamme yeyote yule
baada ya siku ya leo kwa maghiybah [mwanamke aliyekuwa mumewe hayupo] isipokuwa awe pamoja nae mwanamme mwingine au wanaume wawili.” [Imepokelewa
na Muslim, katika Kitabu cha Salaam, mlango uharamu wa kukaa faragha na
mwanamke asiyekuwa maharimu wako na kuingia nyumbani kwake, Hadiyth
namba 4046.].
Hadiyth
hizi za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ziko wazi
katika kutufahamisha kuwa ni haramu kukaa faragha mwanamme na mwanamke
wenye uwezo wa kuoana na kwenda au kuingia katika nyumba ambayo mume
hayupo.
Dada
yangu Muislamu huu pia ni uwanja mwengine wenye kufanywa mwepesi
kufikiwa na kila mtu kwa madai tofauti yakiwemo ya kuwa ni mwenzangu
katika kazi, au ni mwanafunzi mwenzangu, au mengineyo.
Hivyo
ni wajibu kwa mwanamke Swaalihah (mwema) kutomruhusu kuingia katika
nyumba yake isipokuwa yule anayemridhia mumewe wakati yupo huyo mume, na
atakaporuhusiwa iwe kukaa kwake kwa vidhibiti vya kishari’ah; ikiwemo
kutokaa naye faragha au kukaa naye bila ya kuvaa hijabu ya kishari’ah;
au bila ya haja yenye kukubalika; hivyo haitakiwi kukaa pamoja na
asiyekuwa maharimu yake [hata akiwepo mumewe au akiwepo mmoja kati ya
maharimu zake] kwa kuzungumza tu na kuhadithiana yaliyopo au habari
zilizopo.
Kinachojitokeza
siku hizi [ambacho hakikubaliki pia] ni kwa wanawake kukaa faragha na
wasiokuwa maharimu zao kwa kisingizio kuwa wako watoto wao wa kiume
wadogo wadogo [wasio kuwa baleghe], hivyo hudai kuwa faragha imetoweka
kwa kuwepo hao watoto wake wadogo; hii si sahihi, kwani kuwepo
kwa mtoto mdogo na kutokuwepo ni sawa, kwani hakuna anayewaonea hayaa
kwa sababu ya umri wao mdogo; na katika yanayofanywa pia ambayo
yanakwenda kinyume na mafundisho ya Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na kuwa miongoni mwa jumla ya yasiyokubalika
katika Uislamu ambayo ni miongoni mwa namna fulani ya kukaa faragha kwa
mwanamke na asiyekuwa maharimu wake, ni huku kwa baadhi ya watu [wenye
kujiita au kuitwa mustaadh] kwenda kuwaombea [kuwazinguwa] wasichana
wanaotarajiwa kuolewa au kuwasomea mabibi arusi huku wakiwa wamepambika
kisawa sawa, ukaaji wa aina hii kwa hali yoyote ile ikiwa hakuna
maharamu ni ukaaji faragha wa wanaume wengi na mwanamke mmoja pia
hakukubaliki.
Ama
mwanamme akimkuta mwanamke aliyepotea njia, itajuzu kwake kufuatana
naye kwa vidhibiti vya kishari’ah, miongoni mwake ni kwa yule mwanamke
kuwa nyuma ya yule mwanamme katika kwenda kwao na si kwenda sambamba au
bega kwa bega huku wakizungumza na kucheka kama mke na mumewe.
Katazo La Kusalimiana Na Wanaume Kwa Kuwapa Mikono
Kama
ilivyoeleweka kuwa si kila mtu anaruhusiwa na kukubaliwa kusalimia na
kupeana mkono na Malkia; basi hivyo hivyo kwa mwanamke Muislamu ni
malkia mwenye hadhi yake aliyopewa na Muumba wake, hadhi yenye kupita
ile aliyojipandikiza nayo Malkia yeyote yule katika dunia; hivyo basi si
kila mwanamme huruhusiwa kuugusa mkono wake na yeye mwanamke Muislamu
asiwe wa kunyanyua na kunyoosha mkono wake wenye hadhi ya aina yake na
kumnyooshea kila mwanamme.
Uislamu
umeweka kanuni ya uharamu kwa mwanamme kuugusa mwili wa mwanamke na
kinyume chake; ikiwemo mikono yake kwa kisingizio cha kuamkiana.
Kutoka kwa Ma’qal bin Yassaar (Radhiya Allahu ‘anhu) amesema: Amesema Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Mmoja wenu kutongwa [kudungwa] katika kichwa chake (na katika Riwaayah: (cha mwanamme) kwa makhiytt [msumari au sindano] ya chuma ni bora kwake kuliko kumgusa mwanamke asiyekuwa halali kwake.” [Imepokelewa na Atw-Twabaraaniyy, baqiyyatul Miym, Hadiyth namba 16916].
Kutoka kwa Ummul Muuminiyna ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anhaa) amesema kwamba: “Alikuwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akichukuwa [akikubali bila kushika mikono ya wanawake] Bay‘ah ya wanawake kwa matamshi [maneno] tu kwa Aayah hii: (“Ee Nabii! Watakapokujia wanawake Waumini wanakuahidi ya kwamba hawatamshirikisha Allaah na chochote, wala hawataiba,…” [Al-Mumtahinah 60: 12]);
‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘anhaa) akasema: Haukuwahi kugusa mkono wa
Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) mkono wa
mwanamke yeyote yule isipokuwa mwanamke aliye chini ya milki yake. (Na katika Riwaayah:
“Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
Hakika mimi sisalimiani na wanawake kwa kupeana nao mkono).” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, katika Kitabu cha Tafsiyr
Qur-aan, Suwrat Qul A’uwdhu birabbil Falaq, Hadiyth namba 4907 na 6703;
na Muslim, katika Kitabu cha Al-Imaarah, mlango wa namna ya Bay’ah ya
wanawake, Hadiyth namba 3476 na 3477; na Ibn Maajah, katika Kitabu cha
Swalaah, milango ya nyakati za Swalaah, Hadiyth namba 2870].
Na kutoka kwa Umaymah bint Raqiyqah (Radhiya Allaahu ‘anhaa) amesema kwamba nilikwenda kwa Mjumbe
wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) nikiwa pamoja na
wanawake wenzangu tukambay’i Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi
wa aalihi wa sallam) juu ya Uislamu; tukasema: “Ee
Mjumbe wa Allaah! Tunakuaahidi kuwa hatutomshirikisha Allaah na kitu
chochote, na wala hatutoiba, na wala hatutozini, na wala hatutoua watoto
wetu, na wala hatutoleta uzushi tunaozusha tu wenyewe baina ya mikono
na miguu yetu, na wala hatutokuasi katika ma’aruwf; basi Mjumbe wa
Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: Katika
muyawezayo na msiyoyaweza. Akasema: Wanawake wakasema: Allaah na Mjumbe Wake ni Ar-hamu kuliko nasfi zetu; njoo tukuahadi ee Mjumbe wa Allaah, [wakitaka akamate mikono yao kama ishara ya utii];
Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema:
Hakika mimi sigusi mikono wanawake, kauli yangu kwa wanawake mia ni kama
kauli yangu kwa mwanamke mmoja, au mfano wa kauli yangu kwa mwanamke
mmoja.” [Imepokelewa na Maalik, katika Muwattwaa, Riwaayah ya
Yahya Al-Laythiy, katika Kitabu cha Bay’ah, Hadiyth namba 1781; na
Ahmad, katika Musnad, Musnad Kumi waliobashiriwa Jannah, Musnad ya
Wanawake (Radhiya Allahu ‘anhuna), Hadiyth namba 26383 na 26384; na
At-Tirmidhiy, katika Kitabu cha Ijumaa, milango ya Safari, Hadiyth namba
1522].
Hadiyth
hizi dada yangu Muislamu zinathibitisha na kuweka wazi kuwa haijuzu kwa
mwanamke Muislamu kusalimiana kwa kupeana mikono na mwanamme yeyote
yule asiyekuwa maharimu yake, kwani kugusa ni katika vitangulizi ya faahishah [zinaa], na kama ilivyothibiti kuwa Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Ameandikiwa mwanaadamu sehemu yake katika zinaa [kuzini]; hakuna njia ya kuiepuka; macho mawili yanazini [zinaa] zinaa yake ni kutazama, masikio mawili yanazini [zinaa] yake ni kusikiliza, na ulimi unazini [zinaa] yake ni kunena, na mkono unazini [zinaa] yake ni kugusa, na mguu unazini [zinaa] yake ni hatua zake, na moyo hupata matamanio, na tupu husadikisha (hutenda) au kukadhibisha [huacha].” [Imepokelewa Al-Bukhaariy, katika Kitabu cha Tafsiyr Qur-aan, Suwrat Qul A’wudhu birabbil Falaq, Hadiyth namba 6152; na Muslim, katika Kitabu cha Qadar, mlango wa imeandikwa juu ya mwanaadam sehemu yake katika zinaa, Hadiyth namba 4808 na namba 4809].
Kinachojitokeza
siku hizi [ambacho hakikubaliki kabisa katika Uislamu] katika furaha au
msiba ni kwa mwanamke kukumbatiana au kubusiana na wasiokuwa maharimu
zao na wakati mwengine haya hutokezea mbele ya waume zao au kwa ruhusa
ya wamume zao, kwani na yeye
mume hujipatia fursa ya kumbusu au kumkumbatia mke wa mtu mbele ya mkewe
kwa kisingizio kuwa ni tamaduni na njia za kisasa za kimaendeleo za
kufikisha ujumbe wa kusalimiana na kuamkiana zenye kuonyesha na
kuthibitisha upendo na urafiki wa hali ya juu.
Dada
yangu Muislamu ni vyema uelewe kuwa haya yote hayakubaliki katika Dini
unayoifuata kwa ridhaa yako bali yamekatazwa na yote yale yenye
kutangazwa na kuenezwa au kuonekana na wenye kudai kuwa ni wenye kutetea
haki za wanawake au maendeleo ya wanawake na kuwa kuamkiana au
kusalimia kwa kupeana mikono au kukumbatiana na kubusiana baina ya
mwanamke na mwanamme asiyekuwa maharimu yake ni katika alama za urafiki
na maendeleo na kuwa si kweli kuwa kutawapelekea kufikia kwenye faahishah;
madai yao haya na mengine yote ni katika madai ya uongo na yenye lengo
la kupotosha kwani hayana msingi wala dalili yoyote ile kutoka katika
Qur-aan au Sunnah; hivyo dada yangu Muislamu elewa na kuwa na yakini
kuwa mafundisho ya Uislamu yako hapa kwa lengo la kukutunza,
kukuhifadhi, kukuenzi na kukupa hadhi ya aina yake pekee, na moja katika
mafunzo hayo ni kutopeana mikono na mwanamme yeyote asiyekuwa maharimu
yako ni mafundisho sahihi yaliyothibiti katika Sunnah za Mtume wako
Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Katazo La Kusafiri Bila Maharimu
Mwanamke
Muumini na Swaalihah haimpasi kwenda safari bila ya Maharimu wake kuwa
pamoja naye hata ikiwa safari yenyewe ni ya kutekeleza ibada kama vile
ibada ya Hijjah achilia mbali safari ya kutembea au kufanya biashara,
kutalii na kadhalika. Safari ni safari iwe wakati wa Mtume
Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake
(Radhiya Allaahu ‘anhum) au wakati huu wa sayansi na ufundi wa hali ya
juu; na iwe
kwa chombo chochote kile; iwe kwa gari, treni, meli, ndege na
kadhalika; bila ya shaka yoyote ile itakuwa ina mengi ndani yake baadhi yake ni ya hatari na mengine ni ya kashifa, fedheha na dhambi kuyaeleza.
Hekima ya Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kumkataza mwanamke kusafiri peke yake bila ya kuwa na maharimu wake ni ya aina yake pekee, hivyo inawajibika kutekelezwa na kufuatwa na huko ndiko kumtii Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwenyewe, lengo au sababu yake iwe inaeleweka au haieleweki kwa kila mwenye macho, akili na uume kamili [si dayuwth: mwanamme dhaifu asiyejiheshimu na hajali kuhusu tabia chafu ama mavazi mabaya ya wanawake waliko chini yake] na kwa kila mwenye kupenda kuwa miongoni mwa wale wataoingia katika Kauli Yake Allaah:
“Mwenye kumtii Mtume basi atakuwa amemtii Allaah.” [An-Nisaa 4: 80].
Na wala si kuwa miongoni mwa wale watoingia katika Kauli Yake Allaah:
“Basi na watahadhari wanaokhalifu amri yake; isije ikawapata fitnah au [ikawapata] adhabu iumizayo” [An-Nuwr 24: 63].
Katika
hali ya kawaida tu achilia mbali safari mwanamke huhitaji wa kumsaidia,
kumshauri na kubwa kumhurumia kwa anayokutana nayo; na hakuna Arhamu na
mwenye huruma na kuwahurumia wanawake zaidi ya Allaah na Mjumbe Wake
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam); kwani Allaah ni Arhamu kwa
waja Wake kuliko mama kwa mtoto wake, na Mjumbe wa Allaah (Swalla
Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakutumwa isipokuwa awe Rahmah kwa
viumbe vyote wakiwemo wanawake; Allaah Anasema:
“Nasi Hatukukutuma ila ni Rahmah kwa viumbe wote.“ [Al-Anbiyaa 21: 107].
Aliyetumwa kuwa Rahmah kwa viumbe amemkataza mwanamke mwenye kuamini Allaah na Siku ya Qiyaamah kusafiri bila ya Maharimu wake.
Kutoka kwa Ibn ‘Abbaas (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema kwamba Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Asisafiri mwanamke isipokuwa awe pamoja nae maharimu wake, na wala asiingie (katika Riwaayah: Asikae
faragha) mwanamme kwa mwanamke isipokuwa awe na maharimu wake.” Mtu
mmoja akauliza: ee Mjumbe wa Allaah, mimi natarajia kutoka katika jeshi [kwenda vitani] kadhaa wa kadhaa, na mke wangu anatarajia kwenda Hijjah?” Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Akamwambia: Nenda ukahiji pamoja na mkeo.” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, katika
Kitabu cha Hajj, milango ya Muhswar na malipo ya kiwindo, mlango wa
Hajj ya wanawake, Hadiyth namba 1739; na Muslim, katika Kitabu cha Hajj,
mlango wa safari ya mwanamke pamoja na maharimu wake kwenda Hajj,
Hadiyth namba 2801].
Na
kutoka kwa Abu Sa’iyd Al-Khudriyy (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema
kwamba Mjume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
amesema: “Si halali kwa mwanamke anayemwamini Allaah na Siku ya Mwisho kusafiri safari ya [katika Riwaayah: masafa ya siku mbili] siku tatu na kuendelea, isipokuwa awe pamoja nae baba yake, au mtoto wake [aliye baleghe] au mume wake, au ndugu/kaka yake au katika maharimu wake.” [Imepokelewa na Al-Bukhaariy, katika
Kitabu cha Hajj, milango ya Muhswar na malipo ya kiwindo, mlango wa
Hajj ya wanawake, Hadiyth namba 1741; na Muslim, katika Kitabu cha Hajj,
mlango wa safari ya mwanamke pamoja na maharimu kwenda Hajj, Hadiyth
namba 2398 na lafdhi ni lake].
Na
kutoka kwa Abu Sa’iyd Al-Khudriyy (Radhiya Allaahu ‘anhu) amesema
kwamba Mjume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)
amesema: “Asisafiri mwanamke (na katika Riwayah): zaidi ya masiku tatu [siku tatu] isipokuwa awe pamoja na maharimu.” [Imepokelewa
na Muslim, katika Kitabu cha Hajj, mlango wa safari ya mwanamke pamoja
na maharimu kwenda Hajj, Hadiyth namba 2398 na namba 2393].
Katazo La Kuwatazama Wanaume
Allaah
Amewaamrisha wanawake kuinamisha macho yao na wasiwaangalie wanaume
wasio kuwa maharimu zao; Allaah Amesema: “Na waambie Waumini wanawake
wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao.” [An-Nuwr 24: 31].
Imaam
Ibn Kathiyr katika tafsiyr ya Aayah hii amesema: “Na waambie Waumini
wanawake wainamishe macho yao.” kwa yale yote Aliyoyaharamisha Allaah
kutazamwa na wanawake isipokuwa waume zao; ndio Ma’ulamaa wengi wakasema
kuwa: Asili ni kuwa haijuzu kwa mwanamke kuwatazama wanaume wasiokuwa
maharimu zake iwe kwa matamanio au bila ya matamanio.
Na
sababu ya kukatazwa kutazama, ni kwa kuwa wanawake kuwatazama wanaume
au wanaume kuwatazama wanawake ni katika vitangulizi vya zinaa, na
Mjumbe wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) alisema
kuwa kutazama ni katika zinaa ya macho kama ilivyothibiti katika Hadiyth
ya Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu 'anhu) iliyotangulia.
kwa ihsaan ya www.alhidaaya.com
Comments
Post a Comment