KUMI LA MWISHO LA MWEZI WA RAMADHANI

Mwenyezi Mngu Aliyetukuka Ametuwekea ibada tukufu katika kumi la mwisho la Ramadhani, zenye kuzidisha Imani na kufanya ibada zikamilike na neema kutimia. Ibada hizi ni Zaka za Fitri na Swala ya Idi. Ametuwekea Zaka za Fitri ili zimsafishe mwenye kufungana na maneneo machafu na matendo visivyo faa na ni chakula kwa masikini, na Ametuwekea Swala ya Idi ili kudhihirisha nguvu za Waislamu na umoja wao na vile wanavyo jikusanya pamoja.




Lengo la Mada:
  1.   Kuwakumbusha watu fadhla za siku kumi za mwisho wa Mwezi wa Ramadhan
  2. Kubainisha mafundisho ya Mtume katika siku hizi
  3. Kuimarisha mafungamano ya mja na Mola wake, nakufanya bidii kujikurubisha kwa Allah
 
 
Utangulizi
Enyi Waislamu, Siku za mwezi mtukufu wa Ramadhani zinaendelea kuisha. Na hivi karibuni tutaanza kumi la mwisho. Je ndugu yangu Muislamu umejiuliza suali moja; Je nimefaidika kiasi gani na siku zilizopita? Kuwa mkweli na nafsi yako na ujifanyie hisabu ya vitendo vyako kabla hujafika siku ya kufanyiwa hisabu. Ndugu Muislamu, bado wakati upo, na fursa ya kufanya mambo ya kheri bado inaendelea.
Je umijiandaa kiasi gani na umejipangia mikakati gani katika kumi la mwisho?  Kwa hakika ni siku muhimu katika umri wa mwanadamu, nadani yake kuna usiku mtukufu. Mwenye kuafikiwa usiku huo basi amepata kheri ya dunia na akhera. Na mwenye kukosa usiku huo basi amekosa kheri ya dunia na akhera. Ni khasara ilioje mtu kuishi duniani miaka mingi kisha aondoke duniani patupu bila ya kupata kheri ya dunia wala kheri ya akhera. Ndugu Muislamu tafakari na uzingatiae, hujui kama utafika mwakani ili uweze kufunga Mwezi wa Ramadhani.
Watu wema walikuwa wakimuomba Allah mwaka mzima awaafikie kuweza kuzifikia siku hizi za kheri. Na wakifikiwa na siku hizi huwa na furaha nyingi, kwa kupata bahati ya kuishi mpaka  kuweza kufunga Mwezi wa Ramadhani. Ndugu Muislamu Mtume Mohammed (SAW) Ametufundisha mambo mengi na ibada nyingi ambazo Muislamu anaweza kuzifanya kwa ajili ya kujikurubisha kwa Allah (SW). Katika Ibada hizo nikama ifuatavyo:-

Sunna za Kumi la Mwisho:
  1. Kufanya bidii kusali swala ya usiku, na kuwahimiza watu wako nyumbani  kuamka kusali pamoja na wewe. Amesema Mtume (SAW): [ Mwenye kusimama usiku katika mwezi wa Ramadhani kwa Ikhlasi na kutarajia malipo kwa Allah. Atasamehewa madhambi yake yalio tangulia]. Imepokewa katika Sunna ya Mtume (SAW) likifika kumi la mwisho alikuwa akigura matandiko yake na akijitahidi kusimama usiku na kuamsha wake zake na familia yake. 
  2. Kuzidisha juhudi kutafuta Usiku wa cheo. Usiku huu ni bora kuliko miezi elfu moja, bali ni bora kushinda vitu vyote vilivyomo duniani. Mwenye kuafikiwa kupata usiku huu basi kwahakika amefaulu na kupata kheri ya dunia na akhera. Katiak mafundisho ya Mtume (SAW) kuhusu usiku mtukufu; Ni sunna kuzidisha kusoma Qur’ani kwa wingi, kumsifu Allaha na kumtukuza na kumsalia Mtume, kutowa sadaka. Na ni sunna kuomba dua kwa wingi. Bibi Aisha Alimuliza Mtume: Je ni ombe dua gani katika usiku huu? Akamuambia sema: [ Ewe Mola hakika yako wewe ni mwenye kusamehe waja wako na unapenda kusamehe. Nakuomba unisamehe].
  3. Kufanya ibada ya I’tikaaf, nayo ni kutia nia kukaa Msikitini kwa lengo la kujitenga na watu na kukusidia kufanya ibada katika siku hizi. Alikuwa Mtume (SAW) linapo fika kumia la mwisho, akijitenga na familia yake na kuingia Msikitini kwa ajili ya kumuabudu Allah (SW). Na masahaba waliendelea kutekeleza Sunna hii bada ya Mtume kuondoka duniani.
  4. Kusoma Qur’ani kwa wingi na ikiwezekana ku hitimisha Msahafu katika siku hizi tukufu. Imepokewa kutoka kwa Mtume (SAW), ilikuwa ni kawaida yake katika siku za mwezi wa Rmadhani kukutana na Malaika Jibril kwa ajili ya kumsoma Qur’an, na Jibril anamsikiliza.
Ndugu Muislamu, Siku kumi katika kumi la mwisho ni chaguo lake Allah (SW) kwa Umma huu. Na kwa rehma zake Ametujalia sisi kuweza kuzifikia siku hizi tukufu. Kwahivyo, ni jukumu letu kufanya bidii kumuigiza Mtume katika ibada zake zote, na kushindana katika kutafuta Usiku wa cheo (Laylatul Qadri). Tunamuomba Allah Atuajalie miongoni mwa waliochaguliwa kupata Lailatul Qadri (Usiku wa cheo).

Ndugu Waislamu, Allah (SW) Anatupenda sana,  na kwa mapenzi yake juu yetu ni kutujalia malipo na thawabu nyingi kwa kutekeleza ibada ndogo. Mfano Usiku wa cheo ni usiku moja, lakini thawabu zake ni nyingi kushinda thawabu za ibada katika miezi elfu moja. Anglia ndugu Muislamu, utukufu na rehma ya Allah juu yetu, lakini wengi katika Waislmu hawana khabari na neema kama hizi. Wakati unapita, siku zinapita na sisi tume ghafilika, mpaka tutakpo fikiwa na mauti ndio tutazunduka na hali ya kuwa muda umekwisha.
Ndugu Katika Imani, Khasara kubwa zaidi watapata wale waliofanya bidii kufunga mwezi huu na kufanya ibada mwanzo wa Mwezi wa Ramadhani, lakini wanapofikiwa na kumi la mwisho wanarudi nyuma, na kuacha kutekelza ibada na sunna za Mtume (SAW). Ni khasara ilioje kwa mtu aliefanya bidii kuchuma mazuri, kisha akashindwa kuendelea na msimamo huo, na kushindwa kukamilisha kumi la mwisho.
Hukumu ya Ibada ya I’tikaafu:
Ibada ya I’tikafu ni Suuna. Muislamu anaweza kutekeleza ibada hio wakati wowote akitaka. Lakini ni Sunna ilio tiliwa mkazo katika Kumi la mwisho la Mwezi wa Ramadhani.  Amesema Aisha: Mtume (SAW) hakuacha katika maisha yake kufanya I’tikaaf katika kumi la mwisho la Mwezi wa Ramadhan.
 Mambo yanayo lazimu kufanywa katika I’tikaaf:-
a)    Kutia Nia kukaa Msikitini kwa ajili ya kufanya Ibada  kwa lengo la kujikurubisha kwa Allah.
b)    Kuchagua sehemu ya kukaa katika Msikiti,  na kujilazimisha kubaki hapo ila kwa dharura ya kisheria, unaruhusiwa kutoaka.
c)    Kujiepusha na tendo la ndoa au njia za kupelekea kufanya tendo hilo.
d)    Kufanya bidii kuzidisha kusoma Qur’an kwa wingi, na kuomba dua kwa wingi. Kufanya hivyo, itakusaidia kupata usiku wa cheo na kusamehewa madhambi yako.
e)    Kujitahidi kufuata mafundisho ya Mtume katika kutekelez lbada hii.



 Mwisho
Ndugu katika imani, Umri wetu ni mfupi sana, na mwanadamu hajui kama ataweza kupata nafasi tena kufikia mwezi wa Ramadhani mwakani. Jambo la msingi ni kufanya bidii na juhudi kubwa kutafuta Usiku wa cheo ili tupate kheri ya usiku huu. Yule atakaye bahatika kupata usiku huu, kwahakika huyo amefaulu hapa duniani na kesho akhera.
Tunamuomba Allah kwa majina yake matukufu na sifa zake njema atujalie miongoni mwa waja wake  Aliyo wachagua kupata kheri ya Usiku wa cheo. Tunamuomba Allah Atuafikie kwa kufanya Ibada mbalimbali ambazo anazozipenda na anazoridhia. Tunamuomba Allah Atuwezeshe kufuata mafundisho ya Mtume Mohammad katika maisha yetu na atuingize pamoja  na yeye katika Jannatul Firdaws.

Comments

Popular posts from this blog

VIZUIZI 12 VYA KUSHEHEREKEA MAULID

ISEMAVYO QUR-ANI TUKUFU KUHUSIANA NA SWAUMU YA RAMADHANI SWAUMU YA RAMADHANI KATIKA DIRISHA DOGO. ISEMAVYO QUR-ANI TUKUFU KUHUSIANA NA SWAUMU YA RAMADHANI:

AJALI MBAYA YA BASI YATOKEA KAHAMA