UTWAHARA WA MGONJWA
KHUTBA YA KWANZA
Utangulizi
Ewe Muislamu,
Mola amekuumba na atakupa mitihani, basi utakapopata mitihani hiyo
usisahau ibada Yake kama kawaida, tena haswa ibada ya swala.
Utwahara wa Mgonjwa na Swala zake
Baada ya himidi na swala na salamu, Enyi watu,
muogopeni Mwenyezi Mungu kisawa sawa. Ewe muislamu, ujuwe Mola
alituafikia, mimi na wewe tupate kheri ya Uislamu na bila shaka, maadamu
ni Waislamu tutapata mitihani kila aina, ya siri na ya dhahiri ili
tumtambue, tumshukuru na kusubiri. Na ndio Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa
Taala) akasema katika maana ya Aya:
يقول الله جلّ وعلا: {وَلَنَبْلُوَنَّكُمْ حَتَّى نَعْلَمَ الْمُجَاهِدِينَ مِنْكُمْ وَالصَّابِرِينَ وَنَبْلُوَ أَخْبَارَكُمْ ﭨ} [محمد:31].
{{Hakika tutawaonja mpaka tujue waumini wa kweli na wavumilivu miongoni mwenu}}.
Mwanafunzi wa Mtume, Suhaib Ar-Rumii amesema kwamba Mtume
(Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amesema: [Ajabu ni ya huyu Muislamu,
kwa kuwa kila jambo lake ni nzuri. Akipata la kumfurahisha atashukuru na
ni kheri kwake, na akipata la kumuudhi atavumilia na ni kheri kwake].
Amepokea hadithi hii Muslim. Kwa hivyo, Muislamu atavumilia na ataridhike alivyomuahidi Mola.
Allah (Subhaanahu wa Taala) Amesema katika maana ya Aya:
قال تعالى{إِنَّمَا يُوَفَّى الصَّابِرُونَ أَجْرَهُمْ بِغَيْرِ حِسَابٍ ﰙ} [الزُّمَر: 10]
{{ Hakika
watalipwa wavumilivu malipo mengi pasi kuwa na hesabu}}. Bishara njema
kutoka kwa Allah (Subhaanahu wa Taala) kwa wenye kuvumilia na kusubiri.
Amaesema Allah (Subhaanahu wa Taala):
قال تعالى{وَبَشِّرِ الصَّابِرِينَ ﭭ الَّذِينَ إِذَا أَصَابَتْهُمْ مُصِيبَةٌ قَالُوا إِنَّا لِلَّهِ وَإِنَّا إِلَيْهِ رَاجِعُونَ ﭸ أُولَئِكَ عَلَيْهِمْ صَلَوَاتٌ مِنْ رَبِّهِمْ وَرَحْمَةٌ وَأُولَئِكَ هُمُ الْمُهْتَدُونَ َﮃ} [البقرة:157:155]
{{Tena wape
habari njema wavumilivu, ambao wakipatwa na msiba husema, hakika sisi ni
wa Allah kwa hakika sisi kwake yeye tutarejea, hao watapata msamaha na
rehma kutoka kwa Mola wao na wao ndio waongofu}}.
Na katika Hadithi, Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) anasema: [Muumini akikumbwa na shida yoyote, huzuni na kadhalika, hata kudungwa na mwiba, yote humfutia madhambi].
Mja hapendelei Mitihani
Mja hatakikani
apende mitihani wala apatikane na shida yoyote kwa sababu hajui ataweza
kuvumilia au la. Kwa hivyo Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam)
alimjibu Ammi yake ‘Abbas alipomuomba amuombee dua, Mtume akamwambia: [Ewe Ami, omba Mungu akupe afya, na akamkariria hilo]. Habari nyingine kutoka kwa babake Mu’adh Ibn Rafai anasema kuwa alisimama Abu Bakar Swiddiq akihutubu kisha akalia akasema: Mtume
alisimama katika mimbari hii akahutubu kisha akalia akawa anatuambia:
[Muombeni Mungu msamaha na afya kwani hakuna kitu muhimu baada ya imani
na yakini isipokuwa ni afya na kila wakati mja atake msamaha na Mola
ampe afya].
Ewe Muislamu,
ukiwa na afya yako jikurubishe kwa Mwenyezi Mungu vile utakavyoweza na
siku ukiwa mgonjwa akashindwa kufanya kama ulivyokuwa ukifanya basi
fanya utakavyoweza na Mola atakulipa kama ulivyokuwa ukifanya ulipokuwa
mzima, kama vile swala ya mgonjwa na swala ya msafiri.
Umuhimu wa Swala na Uwajibu wa Kuitunza
Enyi waja wa
Allah, Mwenyezi Mungu (Subhaanahu wa Taala) amesema katika maana ya Aya:
“Hakika swala ni lazima kwa muumini kwa wakati niliopanga” na Mtume
akawaeleza kwa uwazi zaidi. Ewe Muislamu hakika tabia ya muumini ni
kuifanya umuhimu wa swala kwa wakati vile alivyotufundisha Mtume (Swalla
Llahu ‘alayhi wasallam). Allah (Subhaanahu wa Taala) Anasema:
قال تعالى: {الَّذِينَ هُمْ عَلَى صَلَاتِهِمْ دَائِمُونَ ﮒ} [المعارج:23].
{{Waja wema ni
wale wanaofululiza swala zao pasina kuacha}}. Kwa hivyo, swala iwe ndani
ya moyo wa muumini, afuzu nayo na ajisikie nayo, na maadamu akili yake
ni nzima basi anaamrishwa kuswali kwa vyovyote vile kama Mola
alivyomuamrisha Mtume Issa Ibn Mariam, alimuamrisha kuswali na kutoa
Zaka maadamu yuko hai.
Jitahadhari na Wenye kudharau Swala.
Ewe Muislamu,
baadhi yetu wanaacha swala sio kwa sababu ya uvivu, bali dunia imeingia
ndani ya nyoyo zao mpaka wakati ukapita, tena sana. Ikiwa mtu ni
mgonjwa ni ajitahidi kuswali kwa hali yoyote mpaka apoe maradhi, na
akipoa ataswali kama mwenye afya yake.
Utwahara kwenye Swala ni lazima.
Hili ni jambo
lililo maarufu na ya kuwa utwahara kwenye swala ni lazima, katika nguo
utakazoswalia na mwili wako wakati ule unaswali na mahali unaposimama
kuswali. Mola (Subhaanahu wa Taala) Anasema katika maana ya Aya:
قال تعالى: {وَثِيَابَكَ فَطَهِّرْ ﯘ} [المدَّثر:4]
{{ Na nguo zako, ewe Muhammad, uzitwahirishe}}.
Mtume
(Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) alikuwa akitembelea makaburini
akateremshiwa wahyi ya kuwa makaburi mawili kati ya hayo waliomo ndani
wanaadhibiwa, kosa la mmoja wao alikuwa hamalizi kujisafisha mkojo na
hamalizi mkojo]. Hadith nyingine Mtume
(Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) amesema: {{ Adhabu wanayoadhibiwa watu
wengi ni kuwa hawamalizi mikojo}}, na Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi
wasallam) amesema [ Haikubaliwi swala ya mmoja wenu ikiwa hana udhu
mpaka atawadhe]. Hivi inamaanisha utwahara wa kila pahali ndio sharia inavyotakikana.
Kujisafisha Magonjwa.
Kujisafisha kwa malengo mawili :-
· Kuwa safi mbele ya viumbe wenzako
· Kuwa safi mbele ya viumbe wenzako na mbele ya Muumba wako.
Kuwa safi mbele
ya viumbe ni kujisafisha choo, mkojo, damu na kadhalika. Na kujisafisha
mbele ya Allah ni kujisafisha hivyo na kutawadha au kuoga au kutayammam.
Kutayamam ni
pale unapokosa maji au ukiwa mgonjwa. Vilevile yawezekana maji yakawapo
lakini ikawa viungo vya udhu vikipata maji utadhurika, ndipo utatayamam,
haya yamesemwa na Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi
wasallam) katika maana ya hadithi ya kuwa: [Ikiwa mnataka kuswali na
hamna maji tayamam kwa mchanga kwani huo pia ni wenye kutwaharisha].
Ewe Muislamu mja
huenda akakumbwa na maradhi kwenye viungo vya udhu, hapo atafuata moja
katika njia mbili:- (1) Atatawadha na pale penye maradhi atapangusa na
aende na udhu wake. (2) Ikiwa hivyo vitamdhuru, basi atatayamamu kama
kawaida. Swahaba Ibn ‘Abbas alisema: ‘Mwenzetu aliyekuwa na kidonda kwa
bahati mbaya alikumbwa na janaba kwa njia ya kuota, wenzetu hawakufahamu
wakamueleza aoge, na swahaba akaoga kidonda kikaingia maji maradhi
yakamzidi na akafa, tuliporejea mjini, Mtume akapelekewa habari ile,
akasema: “Nyinyi mumemuuwa, kama angetayamamu angeendelea kuishi”
Swala ya Mgonjwa.
Ikiwa wewe ni
Muislamu na akili yako inafanya kazi, inafahamu na kuelewa, basi swala
ni juu yako kwa utakavyoweza, ulazima wake sio kama faradhi nyenginezo,
nguzo hiyo iko juu ya mabega yako kwa kila kipindi kikiingia. Ndio
utaona Mtume (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) mwenyewe na maswahaba na
tabiina na waja wema wa kwanza wakitekeleza swala zao kwa afya na
maradhi, Anas Ibn Maalik asema: ‘Siku moja nilipanda farasi, nikaanguka
chini nikaumia, nikaswali kwa kukaa’.
Swahaba mwengine ‘Imran ibn Huswain amesema kuwa yeye alikuwa mgonjwa wa bawasiri akawa ahisi dhiki kusimama na kukaa. Mtume
(Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) akamuambia: [Swali kwa kusimama, ikiwa
huwezi, swali kwa kukaa, ikiwa huwezi swali kwa ubavu. Baadaye Mtume
akaondoka, aliporejea akamkuta anaswali kwa kukaa lakini amekalia mto.
Mtume akakasirika akauondosha ule mto akautupa kando na akasema: ‘Swali
juu ya ardhi ukiweza na kama huwezi swali kwa vyovyote lakini usikose
khushui hata kama utaswali ni kwa kuashiria kwa kichwa katika kurukuu na
kusujudu, ukirukuu utainamisha kichwa kidogo na ukisujudu ndio sana na
iwapo huwezi hivyo, hata ishara ya macho inatosha’. Ama ishara ya
kuswali kwa kidole sio sahihi. Haiko kwenye Qur-an, hadithi wala kwenye
ilimu. Na wala si vizuri ukiwa unaumwa kidogo ukaswali kwa kukalia
kiti, ndipo Misikiti yetu inakaribia kuwa holi kwa viti.
KHUTBA YA PILI
Mgonjwa kuelekea Qibla
Ewe Muislamu,
Hapana budi kuelekea Qibla ili swala ikubaliwe, na hii iko wazi kwa
wanazuoni wote, lakini mgonjwa akiwa hajiwezi na hakupata mwenye
kumsaidia kumuelekeza Qibla na ikiwa kitanda hakikulenga Qibla, ataswali
vile alivyojaaliwa, na wakati mwingine mgonjwa huwa ana najisi au hana
udhu na hakupata mwenye kumsaidia kwa udhu au kumsafisha uchafu,
majeraha yakawa yana damu na usaha, basi ataswali kama alivyojaaliwa.
Habari kutoka kwa swahaba mtukufu, Mansuur ibn Makhramah anasimulia ya
kuwa aliingia nyumbani mwa ‘Umar ibn Khattwab kwa swala ya asubuhi na
‘Umar alikuwa amedungwa na Abuu lu’lu’ah aliyekuwa katika dini ya
kimajusi, lakini ‘Umar alikuwa hajafa bado, majeraha yanamwaga damu na
Khalifa akaendelea na swala kama kawaida. Hivi ndivyo waumini
wanavyokuwa kipindi cha swala hakiwapiti.
Ni wajibu kwa Msimamizi wa Mgonjwa kumsaidia kumtwahirisha na kumkumbusha swala.
Ewe Muislamu,
unaemsimamia mgonjwa nyumbani au hospitalini, Muogope Allah, na ujue ya
kuwa swala ni muhimu, umsaidie mgonjwa wako kwa kumsafisha, umkumbushe
swala na dhikri na zaidi ikiwa ni wazazi wako, kwani wao unapaswa
uwasaidie zaidi kwa kazi hiyo tukufu kama Mola (Subhaanahu wa Taala)
Alivyotuamrisha katika maana ya Aya:
قال تعالى: {وَأْمُرْ أَهْلَكَ بِالصَّلَاةِ وَاصْطَبِرْ عَلَيْهَا ﯖ} [طه:132].
{{ Na uamrishe watu wako swala na uvumilie}}
Ulinganizi kwa Matabibu wamche Mwenyezi Mungu.
Ni sisi Waislamu
tuwaelimishe matabibu kuwa Muislamu ni wajibu aswali na kuwa kuswali
ndio chakula cha roho. Hao matabibu huwapatia dawa wagonjwa kwa vipindi,
nyakati na saa maalumu, tuwakumbushe ilivyo muhimu dawa ya mwili, dawa
ya roho ni muhimu zaidi, haifai kujitukuza wala kudharau. Kila kitendo
kina wakati wake na Mungu aliyetuumba amesema katika maana ya Aya:
والله يقول: {وَتَعَاوَنُوا عَلَى الْبِرِّ وَالتَّقْوَى وَلَا تَعَاوَنُوا عَلَى الْإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ} [المائدة:2].
{{ Saidianeni katika wema na kumcha Mwenyezi Mungu na wala msisaidiane katika madhambi na uadui}}.
Hukumu ya kukusanya Swala Mbili kwa Wakati Mmoja.
Sheria ya
kiislamu imemuhurumia mgonjwa ikamruhusu aswali swala mbili kwa kipindi
kimoja, kwa vile ana shida ya ugonjwa, maumivu ya madawa, kutawadha na
kumsumbua mwenye kumshughulikia, kwa hivyo atakusanya swala ya Adhuhuri
na Alasiri aziswali kipindi cha Adhuhuri au kipindi cha Swala ya
Alasiri. Na swala ya Magharibi na Isha aziswali kipindi cha Magharibi,
au kipindi cha Ishi. Haya yote ni kwa sababu ya kumhurumia mgonjwa.
Nasaha kwa Waislamu Wote.
Ewe Muislamu,
swala iwe ndani ya moyo wako, akili yako roho yako na damu yako, uiswali
kwa wakati wake, na sharti zake. Hakuna litakalo kuachisha Swala
isipokuwa kufa, ili uingie kwenye pepo ya Firdausi iliyo bora kuliko
pepo zote kama vile Mola (Subhaanahu wa Taala) alivyosema katika maana
ya Aya:
قال تعالى: {وَالَّذِينَ هُمْ عَلَى صَلَوَاتِهِمْ يُحَافِظُونَ ﮉ أُولَئِكَ هُمُ الْوَارِثُونَ ﮍ الَّذِينَ يَرِثُونَ الْفِرْدَوْسَ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﮔ} [المؤمنون:11:9].
{{ Waja wema ni
wale wanaohifadhi Swala zao. Hao wataingia pepo ya Firdausi watakaa
humo milele}}. Na hata mkiwa kwenye vita mtaswali kwa kutembea au ikiwa
mmepanda vipando au mtaswali kwa zamu, bora kipindi kiingie, mswali kwa
hali yoyote ile. Namuomba Mwenyezi Mungu atujaalie sisi tuwe waja wema
wenye kutunza swala zetu na hakika yeye kwa kila kitu ni Muweza.
Jueni, Mungu
awarehemu, hakika maneno mazuri ni kitabu cha Mungu na uongofu bora ni
uongofu wa Mtume Muhammad (Swalla Llahu ‘alayhi wasallam) na mambo
mabaya zaidi ni yale yaliozuliwa katika Dini, kwani kila lenye kuzuliwa
huitwa ni uzushi. Kwa hivyo ni juu yenu mshikamane na Sunnah za Mtume na
Maswahaba zake na mumswalie Mtume wenu Muhammad (Swalla Llahu ‘alayhi
wasallam) kwa kufuata amri ya Mola (Subhaanahu wa Taala) wetu Aliposema
katika maana ya Aya:
قال تعالى: {إِنَّ
اللَّهَ وَمَلَائِكَتَهُ يُصَلُّونَ عَلَى النَّبِيِّ يَا أَيُّهَا
الَّذِينَ آَمَنُوا صَلُّوا عَلَيْهِ وَسَلِّمُوا تَسْلِيمًا ﮀ} [الأحزاب:56]
{{Hakika Mwenyezi Mungu na Malaika wake wanamswalia Mtume, Enyi waumini pia nyinyi mswalieni}}.
Ewe Mwenyezi
Mungu, Mswalie na umbariki Mtume Muhammad na watu wake wa kwanza na wa
mwisho na uwe radhi na Maswahaba zake na Makhalifa wake na waliokuja
baada yao mpaka Qiyama.
Mwisho
Ewe mwanadamu
mwenzangu, wewe umeumbwa, hukujiumba, umeletwa hukuletwa, na siku ya
kuondoshwa hutajua. Kwa hivyo ni juu yako kumtwii Allah katika saa
zote, siku zote, wiki zote, miezi yote, miaka yote mpaka mwisho wa umri
wako.
Katika
maisha yako, utapata mitihani ya kila aina, magonjwa na kadhalika.
Ukipatikana na mtihani wa ugonjwa utaswali kama kawaida na ukishindwa
utaswali utakavyoweza, muhimu ni kuwa kipindi cha Swala kisikupite,
maadamu akili yako inafanya kazi, swala imekulazimu. Ewe Mwenyezi Mungu,
Tupe mitihani mipesi ili tusiepukane na Swala.
Comments
Post a Comment