Hii
ni kutokana na mnasaba wa kuingia mwezi
mtukufu wa Ramadhani. Minbari ya
Ramadhani itakuwa ikikuletea mawaidha
yahusiyanayo na funga ya Ramadhani, ili uweze
kuijua funga na hatimaye uweze kufunga kama
alivyoamrisha Mwenyezi Mungu Mtukufu na kama
alivyofunga Bwana Mtume -Rehema na Amani
zimshukie – ambaye ndiye kigezo chetu chema.
Sambamba na Minbari ya Ramadhani, website yako
itakuwa ikikuletea TUNDA LA RAMADHANI.
Kupitia tunda la Ramadhani utajifunza
hadithi mbili tatu za Mtume zihusianazo
na funga tukufu ya Mwezi mtukufu wa
Ramadhani. Hadithi hizi zitakuwa
zikifuatiwa na maelezo mafupi ili kuziweka wazi
kwa wasomaji.
i)
MINBARI YA RAMDHANI NA KHUTBA YA MTUME
KATIKA KUUKARIBISHA MWEZI MTUKUFU WA
RAMADHANI :
Jueni
na eleweni enyi ndugu zanguni Waislamu
kwamba Mwenyezi Mungu Mtukufu amejaalia
mafanikio ya duniani ni ya muda mfupi,
yenye kwisha na kuondoka, na mafanikio ya akhera
ndiyo yenye kusalia/kubakia milele. Haya
mafanikio ya kudumu, hayapatikani ila kwa
kupitia barabara ngumu ya “TAQ-WA”
kumcha Mwenyezi Mungu na kumtii na kumfuata
Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie-. Katika
jumla ya nguzo kuu za Taqwa ni kuufunga huu
mwezi mtukufu wa Ramadhani ambao Allah
ameujaalia kuwa ni REHMA kwa viumbe. Nao kama
mjuavyo ndio mwezi ambao imeteremshwa ndani
yake Qur-ani Tukufu ikiwa ni muongozo
kwa watu wote. Muongozo uliosheheni hoja
wazi za uongofu na upambanuzi baina ya
haki na batili. Ramadhani pia ni mwezi
ambao hufunguliwa ndani yake milango ya
pepo na kufungwa milango ya moto. Ni kwa
kuuzingatia umuhimu na nafasi ya mwezi wa
Ramadhani, ndipo Bwana Mtume akaitoa Khutba yake
tukufu, khutba ya kihistoria, khutba kongwe
katika kuupokea na kuukaribisha mwezi mtukufu wa
Ramadhani.
Imepokelewa
na Salmaan Alfaarisy – Allah amuwie
Radhi – amesema : Alitukhutubia Mtume wa
Mwenyezi Mungu – Rehema na Amani
zimshukie – katika siku ya mwisho ya mwezi wa
Shaabani, akasema : “Enyi watu,
umekufikieni mwezi mtukufu wenye baraka. Ndani
ya mwezi huu umo usiku wa LAYLATIL QADRI usiku
ambao ni bora kuliko miezi alfu moja. Mwenyezi
Mungu amejaalia funga ya mwezi huu kuwa ni
FARADHI na kisimamo (cha ibada) cha usiku wake
kuwa ni SUNA. Atakayejikurubisha (kwa
Mola wake) ndani ya mwezi huu kwa
(kutenda) jambo lolote la kheri,
(malipo, jazaa yake) itakuwa ni kama mtu
aliyetekeleza fardhi katika miezi mingine. Na
atakayetekeleza fardhi katika mwezi huu, atakuwa
ni kama mtu aliyetekeleza fardhi sabini katika
miezi mingine. Na mwezi huu ni mwezi wa SUBIRA,
nao ni mwezi ambao mwanzo wake ni REHEMA
na katikati yake ni MAGHFIRA/MSAMAHA WA
ALLAH na mwisho wake ni KUACHWA HURU NA
ADHABU YA MOTO. Yeyote atakayemfuturisha
mfungaji ndani ya mwezi huu, (ujira wa
futari hiyo) utakuwa ni maghfira ya
madhambi yake (mfuturishaji) na kuachwa huru
na adhabu ya moto na atapata ujira kama aupatao
mfungaji bila ya kupungua chochote katika
ujira/thawabu zake (mfungaji)”. Tukasema :
Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, sio sote tunaweza
kupata (kitu) cha kumfuturisha huyo mfungaji.
(Mtume) akawajibu : “Mwenyezi Mungu humpa
thawabu hizi yule atakayemfuturisha
mfungaji ndani ya mwezi huu kwa
onjo/funda ya maziwa au (kokwa ya) tende
au funda ya maji. Na atakayemshibisha
ndani ya mwezi huu mfungaji, itakuwa
ujira (wa shibe hiyo) ni maghufira ya
madhambi yake (mshibishaji) na Mola wake
atamnywesha katika hodhi (birika) langu funda
moja ambayo hatopata kiu baada yake kabisa. Na
atakuwa na ujira kama aupatao mfungaji bila ya
kupungua chochote katika ujira wake (mfungaji).
Na atakayempunguzia kazi
mtumishi/mfanyakazi wake ndani ya mwezi
huu, Mwenyezi Mungu atamghufiria
madhambi yake na kumuacha huru na adhabu
ya moto. Basi kithirisheni sana ndani ya
mwezi huu mambo manne. Mtamridhisha Mola wenu
kwa kutenda mambo mawili kati ya manne hayo; na
mambo mawili hamjikwasii (hamna budi) nayo. Ama
hayo mambo mawili mtakayoridhisha nayo Mola wenu
ni shahada (kushuhudia kwamba hapana
Mola apasaye kuabudiwa kwa haki ila
ALLAH) na mumtake maghfira. Na ama yale
mambo mawili msiyojikwasia nayo ni
mumuombe Mola wenu pepo na
mjilinde/mjikinge kwake na (adhabu) ya
moto”. Ibn Khuzaymah katika sahihi yake.
MAELEZO
: Ikiwa tunafuatana pamoja, tunaweza
tukaigawa hadithi hii tukufu ambayo ni
khutba kongwe iliyo hai hadi leo na
itaendelea kuwa hai mpaka mwisho wa dunia.
Khutba hii iliyotolewa na Khatibu mahiri, Bwana
Mtume katika kuukaribisha mwezi mtukufu wa
Ramadhani, inagawanyika katika sehemu kuu tatu
au tuseme ina vipengele vikuu vitatu.
Ukiizingatia hadithi utakuta mwanzo wa khutba
yake, Bwana Mtume – Rehema na Amani zimshukie –
anawafahamisha maswahaba na umma mzima
juu ya utukufu, ubora, cheo na nafasi ya
mwezi wa Ramadhani. Kuna hekima/falsafa
gani ndani ya maelezo haya ? Mtume
anauelezea mwezi wa Ramadhani ni mwezi
wa namna gani ili muislamu aujue, kwani
waswahili husema asiyekujua hakuthamini.
Akishaujua atauthamini na kuupa hadhi
yake unayostahili. Kuuthamini na kuupa
heshima mwezi wa Ramdhani ni kuzidisha sana TWAA
kwa Mwenyezi Mungu kwa kufanya namna mbali mbali
za ibada na mambo mengine ya kheri.
Sehemu
ya pili ya hadithi, Bwana Mtume anataja
fadhila/faida na ubora wa mwezi wa
mtukufu wa Ramadhani na kuwa ibada yeyote
inayofanywa ndani ya mwezi huu hailingani
kithawabu/kiujira na ile ibada inayofanywa
katika miezi mingine. Kwa hiyo basi, Ramadhani
ni ndio musimu wako wa ibada. Kadhalika Bwana
Mtume anatuelezea malipo na thawabu adhimu
anazozipata mja mwenye kumfuturisha nduguye
muislamu katika mwezi huu wa Ramadhani. Hapa
Bwana Mtume anaashiria moyo wa ukarimu
na upendo utakiwao waislamu wajipambe na
kuwa nao. Kwani waislamu wakipendana
watakuwa ni wamoja na mshikamano, na
wakishikamana watautawala ulimwengu na
hapatakuwa na nguvu ya kuwashinda, si
magharibi wala mashariki.
Kisha
ndipo Bwana Mtume akaikhitimisha
khutuba yake kwa kutoa wito muhimu kwa
waislamu. Akawataka wakithithirishe sana
kumpwekesha Mola wao kwa kuleta kalima ya
shahada na wamtake sana maghfira. Hali kadhalika
akawataka waislamu wakithirishe mno kumuomba
Mola wao pepo na wamuombe awakinge na moto wa
jahanamu. Ili kuutekeleza wito huu ndipo
wanazuoni wetu wema -Allah awarehemu-
wakatuwekea uradi uletwao msikitini ndani ya
mwezi wa Ramadhani. Chimbuko la uradi huu ni
ile sehemu ya mwisho ya hadithi. Uradi
wenyewe ni huu :
ASH-HADU
AN LAA ILAHA ILLA-LLAHU
NASTAGHFIRULLAH, NAS-ALUKAL-JANNATA WANA’UDHU
BIKA MINAN-NAAR ALLAHUMMA INNAKA AFUWWUN,
TUHIBBUL-AFWA FA’FU ‘ANNAA YAA KARIIM
Tunashuhudia
kuwa hapana Mola apasaye kuabudiwa kwa
haki ila Allah, Tunakuomba maghfira
(msamaha wa madhambi) Ewe Allah,
Tunakuomba pepo na tunajikinga kwako na moto,
Ewe Allah, wewe mimi ni msamehevu na unapenda
msamaha, basi tusamehe Ewe KARIMU.
Haya
shime ndugu zanguni waislamu,
tukithirishe kuuleta uradi huu ndani ya
mwezi wa mavuno; mwezi mtukufu wa Ramadhani.
Kwa kufanya hivyo tutakuwa tumeuitikia wito wa
Bwana Mtume kwa maslahi na faida yetu wenyewe.
TUNDA LA RAMADHANI :
Karibu
ndugu yangu muislamu katika bustani ya
Bwana Mtume -Rehema na Amani zimshukie –
uchume utakavyo na kula kiasi chako
matunda matamu, mazuri yasiyokwisha hamu;
matunda ya Ramadhani. Ili ufaidike na kunufaika
na matunda haya unatakiwa uingie ndani ya
bustani hii tukufu kwa unyenyekevu, utulivu,
adabu, heshima na usikivu.
TUNDA LA KWANZA – DUA YA KUFUTURU
Amepokea
Ibn Majah kutokana na hadithi ya
Abdillah Ibn Amri (amesema Mtume) : YUNA
MFUNGAJI WAKATI WA KUFUTURU KWAKE DUA
ISIYOREJESHWA (yenye kujibiwa bila ya
kipingamizi)”. Ni kwa sababu hiyo ndiyo
Mtume alikuwa akisema (wakati wa kufuturu) :
[ALLAHUMMA
INNIY LAKA SWUMTU WA'ALAA RIZQIKA
AFTWARTU FAGH-FIRLIY MAA QADDAMTU WA MAA
AKHARTU DHAHABAD-DHWAMAU
WABTALLIT-'URUQU WATHABATAL AJRU IN-SHAALLAHU
TAALA]
Maana
yake : “Ewe Mola wa haki ni kwa ajili
yako tu nimefunga na nimefuturu kwa
riziki yako. Basi (nakuomba) unisamehe
dhambi zangu zilizotangulia na zijazo.
Kiu kimeondoka na mishipa imelowana na ujira
umethibiti pindipo atakapo Mwenyezi Mungu
Mtukufu”
Haya
shime ndugu zanguni waislamu, tumuige
Mtume wetu katika hili na mengineyo ili
tutengenekewe duniani na akhera.
Usikubali kuipoteza fursa hii adimu ya
kukubaliwa duao, omba na Mola Karimu atakupa.
TUNDA LA PILI : FADHILA ZA KUHARAKIA KUFUTURU :
Imepokelewa
hadithi kutoka kwa Abuu Hurayrah –
Allah amuwie Radhi – amesema, Amesema
Mtume wa Mwenyezi Mungu – Rehema na
Amani zimshukie- “AMESEMA MWENYEZI MUNGU :
HAKIKA WAJA WANGU WAPENDEZAO SANA KWANGU NI WALE
WAHARIKIAO KUFUTURU” Ahmad na Tirmidhi.
MAELEZO
: Ni vema mtu akafanya haraka kufuturu,
maadam ana uhakika wa kutua/kuzama kwa
jua. Ikiwa hana uhakika, basi ni vema
akasubiri adhana ili asije akafuturu
kabla ya muda. Haya zingatia upendwe na Mola
wako
|
|
Comments
Post a Comment