MWAKA MPYA WA KIISLAM NA HUKUMU YA KUSHEHEREKEA

 
Tayari Waislamu tumeingia kwenye mwaka mpya wa Kiislam wa Hijriyah. Sasa ni vipi tuukaribishe mwaka huu wetu mpya? Na nini umuhimu wake kwetu? Na nini hukumu ya kusherehekea?

KUHESABIKA MWAKA MPYA
Miaka yetu ya Kiislam imeanza kuhesabika baada ya  kuhama (Hijrah)  kwa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  na Maswahaba kutoka Makkah kuhamia Madiynah. Baada ya kuhama, 'Umar (Radhiya Allaahu 'anhu)   akatoa shauri kuwa kwa vile ni mara ya mwanzo wanahamia katika mji ambao wataanza kutumia sharia’h ya Kiislam, basi ni bora kuanza kuhesabu miaka kwa kuanzia mwezi huo waliohama, nao ni mwezi uliojulikana kama Muharram. Na pia inasemekana kuwa 'Umar (Radhiya Allaahu 'anhu) alikuwa akipata barua kutoka kwa mabalozi wake wa nchi mbalimbali zilizokuwa chini ya Uislam, na zilikuwa zikiandikwa majina ya miezi bila tarehe. Akawashauri Maswahaba wenzake kuwa kuwe na tarehe. Wako waliopendekeza tarehe zianze kwa kufuata miaka ya kirumi, na wako waliopendekeza zianze kwa miaka ya kifursi. Mwishowe wakakubaliana ianze pale alipohamia Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) Madiynah.
Na mwaka huu wa Kiislam ambao unafupishwa kama A.H au H kwa kirefu yenye maana ‘After Hijrah’ au Hijriyah, tarehe 1 Muharram H ilikuwa ni sawa na tarehe 16 Julai 622  M. Na ndivyo hivi inavyohesabika mpaka leo.

NINI MAANA YA HIJRAH (KUHAMA)?
Neno 'hijrah' kwa kiarabu mara nyingi linatarjumiwa kuwa ni 'uhamiaji', lakini haina maana tu ni kuhama nchi kwa nchi au mji kwa mji, au maskani kwa maskani, bali ina maana pia 'kuondoka', 'kusogea', 'kuacha', 'kuepukana', 'kujitenga'. Na Qur-aan inatuonyesha kuwa pia ina maana ya kuacha au kuepukana na hali mbaya na kwenda katika hali nzuri japokuwa hakutakuwepo tabu na mashaka.  Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)   
 ((فَآمَنَ لَهُ لُوطٌ وَقَالَ إِنِّي مُهَاجِرٌ إِلَى رَبِّي إِنَّهُ هُوَ الْعَزِيزُ الْحَكِيمُ))  
(((Basi (Nabii) Luutw akamuamini, na akasema (Nabii Ibrahiym): Hakika mimi nahamia katika  (nchi aliyoniamrisha)  Mola wangu, bila shaka Yeye Ndiye Mwenye Nguvu, Mwenye Hikima)) [Al-'Ankabuut: 26]
 
Hayo ni maneno ya Nabii Ibraahiym ('Alayhis-Salaam) kutokana na kauli ya Ibn 'Abbaas na Adh-Dhwahaak, [na kauli nyingine ni maneno ya Luutw 'Alayhis-Salaam] Ibraahiym alipoona kwamba watu wake hawataki kumsikiliza na wameshikilia kubakia katika upotofu na kushindwa kwake kuwafanyia da'awah ndipo alipoamua kuelekea kwa Mola wake Mtukufu. 
Kwa hiyo kuhama vile vile ni alama ya iymaan ya mtu. Na iymaan inahitaji kumkubali Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala)    na kukanusha upotofu. Ina maana kwamba ni kuondoka na kwenda au kuingia katika njia mpya kabisa itakayofanya hali ya mtu iwe bora zaidi katika uhusiano wake na Mola wake. Na hivyo tunaweza kusema kuwa Iymaan ni:
  • Hijrah Kutoka katika kila aina ya shirk na kuingia katika Tawhiyd.
  • Hijrah Kutoka katika ujinga na kuingia katika nuru ya elimu.
  • Hijrah Kutoka katika faragha na kutumia wakati kwa ajili ya Allaah (Subhaanahu  wa Ta'ala)        
  • Hijrah Kutoka katika madhambi, upotofu na kuingia katika twaa ya Mola Mtukufu.
  • Hijrah Kutoka katika kutengana, kuzozana, kupigana, kuchukiana na kuingia katika umoja, usalama, maelewano  na  mapenzi na Waislam.
  • Hijrah Kutoka katika ghadhabu za Mola Mtukufu na kuingia katika Ridhaa Yake.
  • Hijrah Kuepukana na moto ili kupata Pepo ya milele. 
  • Hijra ni hali kamili ya usalama katika Uislam. Inamjenga Muislam kutoka Muumini kuwa ni 'Mujaahid' (mwenye kufanya jihaad) kwa Iymaan yake. Na ndio maana tunaona katika Qur-aan aya nyingi zinataja neno Iymaan, Hijrah na Jihaad pamoja.              
 ((إِنَّ الَّذِينَ آمَنُواْ وَالَّذِينَ هَاجَرُواْ وَجَاهَدُواْ فِي سَبِيلِ اللّهِ أُوْلَئِكَ يَرْجُونَ رَحْمَتَ اللّهِ وَاللّهُ غَفُورٌ رَّحِيمٌ))
((Hakika wale walioamini na wale waliohama na wakapigania Njia ya Mwenyezi Mungu, hao ndio wanaotaraji Rahma za Mwenyezi Mungu. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe na Mwenye kurehemu)) [Al-Baqarah: 218]
((وَالَّذِينَ آمَنُواْ وَهَاجَرُواْ وَجَاهَدُواْ فِي سَبِيلِ اللّهِ وَالَّذِينَ آوَواْ وَّنَصَرُواْ أُولَئِكَ هُمُ الْمُؤْمِنُونَ حَقًّا لَّهُم مَّغْفِرَةٌ وَرِزْقٌ كَرِيمٌ))  
((Na walioamini wakahama na wakapigana Jihaad katika Njia ya Mwenyezi Mungu, na waliotoa mahala pa kukaa na wakanusuru, hao ndio Waumini wa kweli. Watapata msamaha wa Mwenyezi Mungu na kuruzukiwa kwema))
[Al-Anfaal: 74]

((الَّذِينَ آمَنُواْ وَهَاجَرُواْ وَجَاهَدُواْ فِي سَبِيلِ اللّهِ بِأَمْوَالِهِمْ وَأَنفُسِهِمْ أَعْظَمُ دَرَجَةً عِندَ اللّهِ وَأُوْلَئِكَ هُمُ الْفَائِزُونَ))
(( يُبَشِّرُهُمْ رَبُّهُم بِرَحْمَةٍ مِّنْهُ وَرِضْوَانٍ وَجَنَّاتٍ لَّهُمْ فِيهَا نَعِيمٌ مُّقِيمٌ)) 
 ((خَالِدِينَ فِيهَا أَبَدًا إِنَّ اللّهَ عِندَهُ أَجْرٌ عَظِيمٌ))   
((Wale walioamini, na wakahama, na wakapigana Jihaad  katika Njia ya Mwenyezi Mungu kwa mali yao na nafsi zao, hao wana cheo kikubwa zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu. Na hao ndio wenye kufuzu)) 
((Mola wao Mlezi Anawabashiria Rahma zitokazo Kwake, na radhi, na Bustani ambazo humo watapata neema za kudumu)) 
((Watadumu humo milele. Hakika kwa Mwenyezi Mungu yapo malipo makubwa)) [At-Tawbah: 20-22]
Ndugu Waislam, tumekosa fursa ya thawabu za kufanya Hijrah pamoja na Mtume wetu mpenzi (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wakati alipokuwa hai na Maswahaba zake, lakini kuna aina nyingine ya Hijrah ambayo itatupatia thawabu maradufu. Nayo ni kuhama katika yote yaliyoharamishwa na kuingia katika yote yaliyo halali. Tunaona wakati alipoulizwa Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba, "Je, Hijrah gani iliyo bora?" Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) akajibu:   
 (( أن تهجر ما كره ربك عز وجل))  صحيح ألألباني - المصدر النسآءي
((Ni kuhama yale Anayochukia Mola wako Mtukufu ((Swahiyh Al-Albaaniy kutoka An-Nasaaiy   
Na thawabu hizo ambazo usawa wake na Hijrah pamoja  na Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  anaweza kuzipata mtu atakapokuwa katika twaa wakati wa fitnah, nao ni kama wakati wetu huu uliojaa fitnah, kwa hiyo anapojikaza mtu na kujiepusha na fitnah hizo bila shaka atakuwa amepata fadhilia hizo za Hijrah iliyokusudiwa:
 عنْ مَعقِلِ بن يسارٍ ، رضي اللَّه عنْهُ ، قَالَ : قال رَسُولُ اللَّهِ صَلّى اللهُ عَلَيْهِ وسَلَّم :((العِبَادَةُ في الهَرْجِ كهِجْرةٍ إلَيَّ )) رواهُ مُسْلمٌ
 Kutoka kwa Mu'qil bin Yasaar (Radhiya Allaahu 'anhu)   ambaye amesema: Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Ibada katika fitnah ni kama Hijrah kuelekea kwangu)) [Muslim]
 Vile vile kasema:
عن ‏‏عبد الله بن عمرو ‏عن النبي ‏ ‏صلى الله عليه وسلم ‏ ‏أنه قال : ‏‏((المسلم من سلم المسلمون من لسانه ويده والمهاجر من هجر ما نهى الله عنه)) احمد
Kutoka kwa 'Abdullaah bin 'Amru kwamba Mtume (Swalla Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Muislam ni yule mwenye kuwapa amani Waislam wenzake kwa ulimi wake na mikono yake na Muhaajir (mwenye kuhama) ni yule mwenye kuhama (kujitenga) na yale Aliyoyakataza Allaah)) [Ahmad]
Basi na tujiepusha na yote Aliyoyakataza Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na kuzidisha ibada kwa wingi khaswa katika miezi mitukufu kama hii au nyakati tukufu ambazo kwa neema ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Ametujaalia kuwa nazo zikitupitia mwaka mzima, bali kila siku Muislam anaweza kujichumia thawabu nyingi akipenda kama Anvyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) :
((وَهُوَ الَّذِي جَعَلَ اللَّيْلَ وَالنَّهَارَ خِلْفَةً لِّمَنْ أَرَادَ أَن يَذَّكَّرَ أَوْ أَرَادَ شُكُورًا))
((Naye Ndiye Aliyefanya usiku na mchana kufuatana kwa nafuu ya anayetaka kukumbuka, au anayetaka kushukuru)) [Al-Furqaan: 62] 

HAIFAI KUSHEREHEKEA MWAKA MPYA
Waislam tumeanzisha na sisi tabia za kusherehekea mwaka mpya wa Kiislam na kufanya tafrija, kupeana pongezi n.k.
Na hii ni kwa sababu Waislam tumekuwa tuna tabia ya kuwaiga makafiri kila wayatendayo, lakini ukizingatia utaona kwamba hatujalazimishwa kuwaiga au kufuata matendo yao, ila ni sisi wenyewe tumejitia katika ujinga huu wa kuwaiga. Ajabu ni kwamba hatujiulizi kwanini wao hawatuigi sisi mila na desturi za  dini yetu?  Ndio unakuta hata tukijitutumua na kudai hatusherehekei sikukuu zao, kama mwaka mpya wao, basi hapo hapo tutataka kutafuta badili ili na sisi tuwe na chetu, na ndio tukaanza kuvumbua sherehe ya mwaka mpya wa Kiislam.
Utakuta baada ya kubaini kuwa Christmas haituhusu na haifai kusherehekea, basi tunatafuta chetu kinachofanana nayo na hapo kukazuka Maulidi ya Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Mashia huko Misri, na tukaongeza na siku zetu za kuzaliwa (birthdays)! Sasa tunaacha kusherehekea mwaka mpya wa Gregorian na tunasherehekea mwaka mpya wa Kiislam. Yote hayo hayakupatikana katika mafundisho ya Mtume wala Maswahaba watukufu, kwanini tunayahitaji leo hii?
Imekuwa ni desturi ya Waislam wengi unapofika mwaka mpya wa Kiislam, hutumiana salaam, maamkizi katika njia mbali mbali kama simu za mkono, barua pepe (e-mail) na kadhalika na kuamkiana kusema 'Hongera za mwaka mpya' (Happy new year) au ‘Kullu Aam Wa-Antum Bikhayr’ na kutumiana kadi kama vile wanavyofanya makafiri katika sherehe zao.
Yote hayo ni mambo ya uzushi na ya kuwaiga makafiri, Na hii inasababishwa na kutojiamini na utukufu wa dini yetu na tuliyoyapokea kutoka kwa Mtume na Maswahaba zake. Tumekuwa tunaona yale ya dini yetu kama hayatoshi na kuna haja ya kuongeza na kujazia sehemu pungufu pungufu (kwa mtazamo wetu). Imefikia leo hii zile nembo za Kiislam, mavazi waliyozoeleka nayo Waislam kuonekana duni na kudharauliwa na Waislam wenyewe. Na kuvaa kimarekani na nguo za mitindo (designers) ndio ustaarabu, maendeleo na kuonekana ni mtu wa jamii na anayekwenda na wakati! Ndio utakuta hata Mayahudi leo hii wamechukua nafasi katika kuzifyonza pesa za Waislam kwa kuwatengenezea mavazi 'yao', kama mabaibui, kanzu, vitambaa vya kichwa n.k. Mfano mzuri ni kampuni ya Kiyahudi itwayo CK (Calvin Klein), madada zetu leo hawaoni Hijaab ila iliyo na jina la CK!!
Mambo hayo yanampasa kila Muislam ajiepushe nayo. Kila mmoja akiacha kusherehekea na kumtumia mwenzie maamkizi ya mwaka wetu mpya ndipo tutakapoweza kusimamisha na kuua mila hizi za kuiga.
Shaykh Muhammad bin Swaalih Al-‘Uthaymiyn alipoulizwa je, nini hukumu ya kupeana hongera kwa mwaka mpya wa Kiislam au kuamkiana na kuombeana du'aa? Akajibu:
"Ikiwa mtu atakupa hongera au kukuamkia, basi muitikie lakini usianzishe wewe kufanya hivyo. Na rai iliyo bora kabisa katika mas-ala haya ni kwamba mtu atakapokuambia: 'Hongera ya mwaka mpya' basi sema: 'Tunamuomba Allaah aufanye uwe mwaka wa kheri na baraka kwako'. Lakini usianzishe abadan wewe kwa sababu sikuona mapokezi yoyote kwamba Salafus-Swaalih (watangu wema) walikuwa wakiamkiana au kupeana hongera katika mwaka mpya wa Hijrah"      
Muislam anapopitisha miaka yake hana maana kuwa ana furaha bali ahesabu kuwa siku zake zinazidi kupungua na kukaribia kuingia kaburini, kwa hiyo iwe ni masikitiko na sio furaha khaswa kwa yule ambaye hakujishughulisha kufanya mema mengi. Miaka itakuwa ni ya kufaulu pindi ikiwa siku zimetumika kwa twaa ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na itakuwa ni ya huzuni ikiwa miaka hiyo itatumika kwa maasi.   
Makafiri pia huweka azimio (resolution) yaani kuweka lengo au malengo atakayoyafanya katika mwaka huo mpya, nayo yote ni mambo ya kidunia, lakini Muumini khaswa haweki lengo lake au malengo yake kila mwaka tu, bali aweke kila siku, na juu ya hivyo sio lengo au malengo ya kidunia bali ni malengo ya kujirekebisha kuwa bora kuliko siku iliyopita. Siku zinatupita, masaa yanatupita na hali za Waislam wengi hazibadiliki kuwa bora kwa wao kujiweka mbali na Mola wao.

UMUHIMU WA MWAKA WA KIISLAM (HIJRI)
Inasikitisha kuona kwamba Waislam tumeudharau kabisa mwaka wetu wa Kiislam (Hijri) kwa kuacha kuutumia kabisa. Ingawa mwaka wa Gregorian ndio unaotumika kwetu katika shughuli za kiofisi kwa miaka mingi, lakini isiwe sababu ya kupuuza mwaka wetu wa Hijri, bali tujitahidi kadiri tuwezavyo kuutumia.
Leo ukimuuliza Muislam mkubwa au mtoto akutajie miezi ya Gregorian atakutajia yote bila ya kukosea, lakini ukimuuliza miezi ya Hijri pengine hata mitatu ashindwe kukutajia.      
Ndugu Waislam, tunawasisitiza kubakia katika mila na desturi zetu, zenye mafundisho yaliyo sahihi kutoka katika Qur-aan na Sunnah, kwani hiyo ndio fakhari yetu  na  kufaulu kwetu kote kunategemea kufuata mafunzo hayo. Inapasa Umma Wa Kiislam uwe tofauti na Ummah mwingine kwa desturi, tabia, mazingira na hali nzima zetu za maisha. 
Tuuepushe Ummah wetu kuwa ni watumwa kwa ajili ya kuwa vipofu katika kuiga. Na kuiga huku hakutotuletea wema au kuzuia uovu, bali kutafanya Ummah Wa Kiislam kuwa zaidi ni dhaifu na kutegemea wengine daima na hii itasababisha hata kusahau neema tulizokuwa nazo Waislam miaka iliyopita.
Ummah hautatengenea ila kwa kufuata njia ile ile ilyotengeneza Ummah kabla. Tumejifunza katika dini yetu kuwa siku inaanza jua linapokuchwa (linapozama) na mwezi unaanza unapoandama na mwaka unaanza siku aliyohama Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na hivyo ndivyo walivyokuwa wakihesabu na kurekodi shughuli zao zote za kihistoria Waislam wa zamani; kuhesabu umri wao, na katika kila njia ya kuamiliana hata katika kuandikiana madeni na kadhalika. Basi na tujaribu na sisi kuzitumia ili kuadhimisha mwaka na  siku zetu za Kiislam.       
Tunamuomba Allaah Atujaalie miongoni mwa wanaosikiliza kauli nyingi na kufuata zilizo njema.

Comments

Popular posts from this blog

VIZUIZI 12 VYA KUSHEHEREKEA MAULID

ISEMAVYO QUR-ANI TUKUFU KUHUSIANA NA SWAUMU YA RAMADHANI SWAUMU YA RAMADHANI KATIKA DIRISHA DOGO. ISEMAVYO QUR-ANI TUKUFU KUHUSIANA NA SWAUMU YA RAMADHANI:

AJALI MBAYA YA BASI YATOKEA KAHAMA